Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Masha Msomba na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama Cha Waajiri (ATE) wakionesha hati za makubaliano.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) , Masha Msomba (kushoto aliyekaa) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama Cha Waajiri (ATE) Bi Suzanne Ndomba Doran (Kulia aliyekaa) wakitia saini makubaliano hayo ya ushirikiano (Memorandum of Understanding -MOU).
Waziri wa Nchini , Ofisi ya Waziri Mkuu , Kazi , Ajira na Mahusiano , Deus Sangu akizungumza kwenye mkutano mkuu wa 67 wa wanachama na kongamano la waajiri nchini lililoandaliwa na Chama cha Waajiri nchini (ATE)
Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama Cha Waajiri nchini (ATE) . BI. Suzanne Ndomba Doran akizungumza na waajiri na wageni waalikwa katika mkutano wa 67 wa wanachama na kongamano la waajiri nchini.
Waziri wa Nchini , Ofisi ya Waziri Mkuu , Kazi , Ajira na Mahusiano , Deus Sangu akisalimiana na katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Hery Mkunda.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Cha Waajiri nchini (ATE) Oscar Mgaya akizungumza kwenye kongamano hilo.
***
👉TUCTA yatoa wito wa ushirikishwaji na ruksa ya wafanyakazi kujiunga vyama ya wafanyakazi
Na Damas Makangale, Dar es Salaam
Ushirikiano wa kimkakati kati ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) unatarajiwa kufungua fursa mpya za kuboresha mfumo wa hifadhi ya jamii kwa waajiri na wafanyakazi katika sekta rasmi na isiyo rasmi, huku ukichochea ukuaji wa biashara na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili, kuongeza uelewa kuhusu masuala ya hifadhi ya jamii na kupanua wigo wa huduma kwa waajiri na wafanyakazi nchini.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 67 wa Wanachama wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na Kongamano la Waajiri nchini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deus Sangu, alisema ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya pamoja ya kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha ustawi wa wafanyakazi.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kusikiliza changamoto zinazowakabili waajiri, ikiwemo malalamiko kuhusu tozo na adhabu zilizotokana na malimbikizo ya michango ya wafanyakazi.
"Serikali ya Awamu ya Sita ni sikivu. Nilisikia kilio cha waajiri kuhusu tozo na adhabu zilizotokana na malimbikizo ya michango ya wafanyakazi, hivyo nikaiagiza NSSF kuondoa tozo hizo, hususan kwa waajiri waliokuwa na madeni ya michango," alisema Sangu.
Alisema hatua hiyo imewapa nafuu waajiri na kuwawezesha kuelekeza fedha walizokuwa wakizitumia kulipa tozo katika kupanua biashara, kuongeza mitaji na uwekezaji, hatua itakayoongeza uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.
"Hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa waajiri kuelekeza fedha hizo katika kupanua biashara zao, kuongeza mitaji na uwekezaji, hivyo kuongeza uzalishaji na mchango wao katika uchumi kupitia ulipaji wa kodi mbalimbali," alisema.
Waziri Sangu aliwataka waajiri kuendelea kutekeleza matakwa ya kisheria kuhusu kima cha chini cha mshahara, kuheshimu sheria za kazi na kuhakikisha wafanyakazi wanapatiwa mikataba ya ajira inayokidhi matakwa ya sheria ili kudumisha amani na mahusiano mazuri sehemu za kazi.
Aidha, alisema ni muhimu waajiri wakaendelea kuboresha mazingira ya kazi na kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao za hifadhi ya jamii ili kuwawezesha kuwa na maisha yenye uhakika hata baada ya kustaafu.
"Makubaliano ya leo kati ya ATE na NSSF yana manufaa makubwa kwa wafanyakazi wa sekta rasmi na isiyo rasmi. Yanasaidia kuhakikisha wafanyakazi wanajiandaa kwa maisha baada ya kustaafu na kumudu gharama za maisha kupitia mafao yatokanayo na michango yao," alisema.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bi. Suzanne Ndomba Doran, alisema kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kujadiliana, kujenga uelewa wa pamoja na kufikia maamuzi yatakayotekelezwa kwa manufaa ya waajiri na wafanyakazi.
Alisema mfumo imara wa hifadhi ya jamii unapaswa kujenga uwiano kati ya kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuwezesha biashara kukua, kuendelea kuzalisha na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.
"Kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuimarisha hifadhi ya jamii na uendelevu wa biashara kupitia ushirikiano wa kimkakati, kurahisisha kanuni na kuunganisha mifumo ya taasisi."
"Kauli mbiu hii inatukumbusha jambo moja muhimu kwamba ustawi wa mfanyakazi na mafanikio ya biashara ni mambo yanayokwenda sambamba," alisema Bi. Ndomba.
Aliongeza kuwa waajiri wanaunga mkono mfumo bora wa hifadhi ya jamii kwa sababu mfanyakazi mwenye usalama wa kijamii hupata utulivu wa kufanya kazi, huongeza tija na kuchangia maendeleo endelevu ya taasisi pamoja na taifa.
Bi. Ndomba alisema maeneo muhimu yanayopaswa kupewa kipaumbele ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya waajiri na taasisi za hifadhi ya jamii, kuboresha kanuni na taratibu ili kupunguza urudufu wa huduma, ucheleweshaji na gharama zisizo za lazima.
Alisema ushirikiano huo pia utawezesha taasisi kubadilishana taarifa kwa urahisi, kutumia mifumo ya kidijitali na kutoa huduma kwa wakati.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hery Mkunda, alisema wafanyakazi wanaamini kuwa kuimarishwa kwa mifumo ya hifadhi ya jamii kutasaidia kuongeza usalama wao wa kiuchumi na kuboresha ustawi wao mahali pa kazi.
"Nimefurahishwa na mada kuu ya mkutano wa mwaka huu inayosema Kuimarisha Kinga ya Jamii na Uendelevu wa Biashara kupitia Ushirikiano wa Kimkakati, Kurahisisha Taratibu za Udhibiti na Kuunganisha Mifumo ya Taasisi."
Alisema mada hiyo inasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, waajiri, vyama vya wafanyakazi, taasisi za hifadhi ya jamii na washirika wa maendeleo katika kujenga mazingira wezeshi kwa ukuaji shirikishi wa uchumi.
Mkunda aliwataka waajiri kuendeleza utamaduni wa kuwashirikisha wafanyakazi katika maamuzi yanayohusu sehemu za kazi pamoja na kuheshimu haki yao ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, alisema makubaliano yaliyosainiwa kati ya NSSF na ATE ni ushahidi wa dhamira ya pamoja ya kuimarisha mfumo wa hifadhi ya jamii nchini.
"Ushirikiano huu utachochea ajira zenye staha, kuongeza usajili wa wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kuimarisha biashara pamoja na uwekezaji wenye tija katika sekta binafsi," alisema.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji kupanua wigo wa huduma za hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi wa sekta rasmi na isiyo rasmi ili kuongeza ajira, kukuza sekta binafsi na kuharakisha ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Makubaliano hayo yanatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya waajiri, Serikali na taasisi za hifadhi ya jamii, kwa lengo la kujenga mazingira bora ya kazi, kulinda ustawi wa wafanyakazi na kuendeleza ukuaji wa uchumi wa Tanzania.





