HABARI

SAT, I AM ORGANIC WATOA ELIMU YA KILIMO HAI KWA WAKULIMA, WAJASIRIAMALI NA WAFANYABIASHARA SABASABA

Home
HABARI
SAT, I AM ORGANIC WATOA ELIMU YA KILIMO HAI KWA WAKULIMA, WAJASIRIAMALI NA WAFANYABIASHARA SABASABA

Meneja miradi wa Shirika la kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Bw. Peter Mwangalo, akiwaonyesha wananchi na waandishi wa habari (hawapo pichani) bidhaa mbalimbali zinazotokana na kilimo hai, ambacho huzalisha mazao bila matumizi ya kemikali na mbolea zenye madhara, katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, chini ya uratibu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Meneja miradi wa Shirika la kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Bw. Peter Mwangalo, akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu bidhaa zinazozalishwa kwa njia ya kilimo hai katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayofanyika Dar es Salaam chini ya uratibu wa TANTRADE.
Meneja miradi wa Shirika la kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Bw. Peter Mwangalo akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu bidhaa zinazozalishwa kwa njia ya kilimo hai katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayofanyika Dar es Salaam chini ya uratibu wa TANTRADE.
Meneja wa Duka la I AM ORGANIC, Bi. Dainess Sunday, akitoa elimu kwa wakazi wa Dar es Salaam waliotembelea banda la I AM ORGANIC kuhusu bidhaa za kilimo hai katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wakitembelea banda la SAT na I AM ORGANIC katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Meneja miradi wa Shirika la kilimo Endelevu Tanzania (SAT), Bw. Peter Mwangalo, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kilimo hai katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Dar es Salaam.

***

#SAT na I AM ORGANIC waendelea kuhamasisha kilimo hai kwa Watanzania

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Takribani wakulima 1,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini pamoja na wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) 50 wamejengewa uwezo kuhusu kilimo hai, ambacho hakitumii kemikali na kinachochangia kukuza mnyororo wa thamani kupitia masoko ya bidhaa zinazozalishwa kwa njia salama kwa afya na mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, kwenye banda la Wizara ya Kilimo linaloratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Meneja miradi wa Shirika la kilimo Endelevu Tanzania (SAT) Bw. Peter Mwangalo, amesema maonesho hayo yanawapa Watanzania fursa ya kujifunza kuhusu kilimo hai kinachozingatia kanuni za ikolojia na kutotumia kemikali katika uzalishaji.

Amesema mradi huo unaofadhiliwa na shirika la Bio Vision la Uswisi unaendelea kuwajengea uwezo wakulima pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati ili kukuza mnyororo wa thamani na kufungua masoko mapya ya bidhaa zinazotokana na kilimo hai.

"Mradi huu wa miaka minne una lengo la kuhakikisha wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali wanapata uelewa, mafunzo na mbinu za kufanya kilimo hai bila kutumia mbolea na kemikali zenye madhara kwa afya na mazingira," amesema Bw. Mwangalo.

Ameeleza kuwa kilimo hai kina manufaa makubwa kwa jamii kwa kuwa hutumia mbinu za asili badala ya kemikali na dawa zenye madhara, hivyo kulinda afya za walaji, wazalishaji na mazingira.

Aidha, amewahimiza Watanzania kutembelea banda la Shirika la Kilimo Endelevu Tanzania (SAT) na I AM ORGANIC katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu kilimo hai na kujionea bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kwa kutumia mfumo huo.

Kwa upande wake, Meneja wa duka la I AM ORGANIC, Bi. Dainess Sunday, amesema bidhaa za kilimo hai huzalishwa kwa kutumia mbinu za ikolojia ambazo ni rafiki kwa mazingira, huhifadhi bayoanuwai na kulinda afya za wazalishaji na walaji.

Amesema lengo la mradi huo ni kuendelea kuwajengea uwezo wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali kuhusu umuhimu wa kilimo hai na kuongeza thamani ya bidhaa zake kupitia masoko mbalimbali.

Bi. Sunday amesema matumizi ya bidhaa zinazotokana na kilimo hai yanaweza kusaidia kupunguza hatari ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, yakiwemo baadhi ya saratani, kwa kuhamasisha ulaji wa vyakula vinavyozalishwa bila matumizi ya kemikali hatarishi.


"Tunafungua fursa kwa wakulima wa mazao ya kilimo hai kupata masoko ya ndani na nje ya nchi, huku tukiendelea kutoa elimu kuhusu mchango wa kilimo hai katika kulinda afya za binadamu na kukuza uchumi," amesema.

Naye mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Bi. Aslatu Nguku kutoka Mama Health Organic Shop ya Dodoma, amesema kilimo hai kina mchango mkubwa katika utunzaji wa mazingira kutokana na matumizi ya mbinu rafiki kwa mazingira.

Amesema matumizi ya bidhaa zinazotokana na kilimo hai yanaendelea kuongezeka katika mikoa mbalimbali nchini kadri wananchi wanavyozidi kutambua faida zake kiafya na kimazingira.

Mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na shirika la Bio Vision la Uswisi kwa zaidi ya shilingi bilioni 1.2, ukiwa na lengo la kuwajengea uwezo wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali kupitia mafunzo, taarifa na mbinu bora za uzalishaji wa kilimo hai.

Hadi sasa, mradi huo umefanikiwa kuwafikia wakulima, wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Njombe, Lindi, Iringa, Arusha na Kagera kwa kuwapatia mafunzo na kuhamasisha matumizi ya kilimo hai kwa manufaa ya afya, mazingira na uchumi.

Kilimo hai kinatajwa kuwa miongoni mwa mbinu endelevu za kilimo zinazochangia kuboresha afya za wananchi, kulinda mazingira na kupunguza matumizi ya kemikali zinazoweza kusababisha madhara kwa binadamu na mfumo wa ikolojia.
Previous Posts Next Posts